Siku ya chakula duniani tuazimie kila binadamu anapata mlo bora: Ban

16 Oktoba 2013

Zaidi ya watu Milioni 840 duniani kote humaliza siku bila mlo bora katika ulimwengu huu uliojaliwa rasilimali, ni sehemu ya ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ban Ki-moon katika siku ya chakula duniani hii leo akionyesha kushangazwa na hali hiyo inayopaswa kufanya watu wachukue hatua.

Bwana Ban amesema changamoto ni kubwa zaidi, kwani watu Bilioni Mbili wanakabiliwa na njaa isiyoonekana kwa kukabiliwa na utapiamlo. Amesema lishe isiyo bora inafanya watu wapatao Bilioni Moja na nukta nne wawe na unene wa kupindukia ambapo kati yao wana hatari ya kupata magonjwa ya moyo, kisukari na matatizo mengine ya kiafya.

Amesema jibu pekee ni kuhakikisha kila mtu anapata mlo sahihi kwa kuhakikisha kuna mifumo, sera na uwekezaji bora unaoweka fursa ya mazingira bora na watu kuzalisha mazao bora na salama na kufikia watu kwa uhakika.

Hata hivyo Katibu Mkuu ameeleza kufurahishwa kwake kwani nchi nyingi zimeunga mkono kampeni yake ya kutokomeza njaa ambapo pia zimeahidi kuweka mifumo endelevu ya upatikanaji chakula.