Nyerere alitufundisha kuthamini uhuru: Mwakilishi wa Afrika Kusini

14 Oktoba 2013

Katika kumkumbuka Mwalimu Julius Nyerere mnamo Oktoba 14, Mwakilishi wa Kudumu wa Afrika Kusini kwenye Umoja wa Mataifa, Kingsley Mamabolo, amesema kuwa Mwalimu Julius Nyerere alitoa mafunzo muhimu kwa wanadamu kufurahia na kuthamini uhuru daima.

Akisifu mchango wake kwa ukombozi wa Afrika Kusini kutokana na uongozi wa ubaguzi wa rangi na kwa makundi mengine ya ukombozi kusini mwa Afrika, Balozi Mamabolo amesema kuwa Mwalimu Nyerere alitufundisha kuelewa daima kuwa sote ni sehemu ya ubinadamu, na bila kujali misingi ya rangi, utaifa au dini, hamna mtu ambaye anatakiwa kukubali dhana kuwa kuna watu wa chini na wengine wanaowazidi.

“Julius Nyerere na viongozi wa kizazi chake cha viongozi wa Afrika, walianzisha mapambano dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, na kuendeleza umoja wa kisiasa na kiuchumi kwa bara la Afrika. Na kwa maneno yake, alisema umoja hautatutjirisha, ila utafanya iwe vigumu kwa Afrika na watu wake kupuuzwa na kudhalilishwa. Na utafanya maamuzi yetu kuhusu maendeleo yawe ya kufana zaidi.”

Mwalimu Julius Nyerere alijitahidi kuhakikisha kuwa sote kama jamii ya kimataifa tunafahamu jukumu tulilo nalo kwa pamoja kupigania uhuru, haki, maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kupiga vita umaskini na njaa, na kuufanya ulimwengu mahali bora zaidi pa kuishi.