Uadilifu na ujasiri wa Mwalimu Nyerere ulitupa mwongozo: Eliasson

14 Oktoba 2013

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson, amesema kuwa itikadi, uadilifu na ujasiri wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere uliwapa wengi msukumo na mwongozo wa kutenda wema.

Bwana Eliasson ambaye amekuwa mgeni wa heshima kwenye hafla ya kuadhimisha Siku ya Mwalimu Nyerere, Oktoba 14, ambayo pia ni siku ya kumbukumbu ya kifo chake, amesema alikutana na Mwalimu Nyerere mara kadhaa, na kuongeza kuwa anafurahia alichofanya Nyerere kwani alikuwa daraja kati ya Afrika na bara Ulaya, na kwamba Nyerere alifanya urafiki ulotokana na misingi ya kuheshimiana na uadilifu.

“Rais Nyerere alitoa mafunzo ya kuigwa katika diplomasia, ambayo yalitoa mwongozo kwa kazi yangu binafsi kama mpatanishi. Nimebahatika pia kumrithi mheshimiwa binti wa Tanzania, Dkt Rose Asha Migiro kama Naibu Katibu Mkuu, na mara kwa mara aliwahimiza wanafunzi kuchangia taifa lao kama vile alivyofanya Rais Nyerere.”

Bwana Eliasson amesema Hayati Rais Nyerere alipigania Afrika kujiongoza, bila kumtegemea mgeni, na kumsifu kama mtu wa maono pevu, akili za kipekee, ukarimu na ucheshi.

“Alikuwa mtu wa itikadi, mwenye fikra bunifu na alijihusisha sana kwa ujasiri katika kupambania haki na uhuru. Alifikia kiwango cha juu zaidi katika uongozi wake. Aliamini kuwa ufanisi katika siasa kamwe haupimwi kwa mali alizojilimbikizia mtu, ila katika kujitoa kuwahudumia watu kwa manufaa ya umma. Viongozi kote duniani sasa, wanapaswa kuiga mfano huu wa busara.”