Ban alaani kuongezeka kwa mashambulizi ya bomu Iraq

14 Oktoba 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa BanKi-moon amelaani vikali msururu wa mabomu ambayo yamewaua na kuwajeruhi watu wengi katika siku chache zilizopita nchini Iraq, wakiwemo wanafunzi wa shule.

Bwana Ban ametuma risala za rambirambi kwa familia za wahanga na serikali ya Iraq, huku akiwatakia majeruhi nafuu haraka.

Katika taarifa ilotolewa na msemaji wake, Katibu Mkuu amesema mashambulizi haya ambayo ni sehemu ya ongezeko la mashambulizi ya mara kwa mara yanafaa kukemewa, hasa kwa sababu yanawalenga raia wa Iraq wakati huu wa Siku Kuu ya Eid Al-Adha wanapoonyesha ukarimu wao kuwasaidia watu maskini.

Ametoa wito kwa viongozi wa Iraq kujikita katika kuungana kisiasa na kuinusuru nchi yao ili isitumbukie katika machafuko ya kidini. Amesema Umoja wa Mataifa pamoja na ujumbe wake nchini Iraq, UNAMI, utaendelea kushirikiana na serikali na watu wa Iraq katika kujenga nchi yenye amani, demokrasia na maendeleo.