Boti nyingine yazama mwambao wa Sicily Italia:IFRC

12 Oktoba 2013

Boti iliyokuwa na wahamiaji takribani 250 imezama Ijumaa kwenye mwambao wa Sicily , kilometa 120 kutoka kisiwa cha Lampedusa kwenye eneo la bahari ya Maltese nchini Italia. Kwa mujibu wa shirikisho la kimataifa la chama cha msalaba mwekundu na mwezi mwekundu IFRC taarifa za awali zinasema watu wapatao 34 wamepoteza maisha na shirikisho lilo limeongeza kuwa linaendelea kuwasiliana na chama cha msalaba mwekundu cha Italia ili kutoa usaidizi wowote utakaohitajika. Kufuatia tukilo hilo la Rais wa chama cha msalaba mwekundu nchini Italia Francesco Rocca amezitolea wito serikali kuhakikisha ulinzi na usalama wa wale wote wanaokabiliwa na safari za baharini kuelekea Ulaya ambapo wengi wao wanakimbia hali za machafuko kama Somalia. Taarifa zinasema Ijumaa hiyo hiyo pia boti nyingine ilizama katika mwambao wa Alexandria Misri na watu 12 kupoteza maisha wengi wakiwa ni wakimbizi wa Syria. Matukio haya yanafuatia zahma ya wiki iliyopita ambapo wahamiaji zaidi ya 300 walipoteza maisha baada ya boti kuzama pwani ya Lampedusa. IFRC imerejea wito kwa serikali zote kuwalinda wahamiaji na utu wao  na kuzingatia sheria za kimataifa za kutoa ulinzi kwa whamiaji na kuhakikisha wanapata huduma za haraka za kibinadamu kama za afya, malazi na kuwasiliana na familia zao.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter