Baraza la usalama laridhia jopo la pamoja la OPCW-UM nchini Syria, Ban azungumza

11 Oktoba 2013

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeridhia jopo la kwanza kabisa la Umoja wa Mataifa na mshindi wa tuzo ya amani ya nobel mwaka huu, OPCW ambalo ni shirika la kimataifa la kupinga matumizi ya silaha za kemikali. Jukumu la jopo hilo ni kusimamia kazi ya kuteketeza na kuharibu mpango wa silaha za kemikali wa Syria ikiwemo silaha na mitambo ya uzalishaji.

Katika barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, Baraza la Usalama limeridhia mpango wa kupeleka wataalamu wapatao 100 wa OPCW na Umoja wa Mataifa katika operesheni za awamu kwa ajili ya kutekeleza azimio la mwezi uliopita la baraza hilo kuhusu Syria, kazi inayopaswa kumalizika tarehe 30 Juni mwaka 2014.

Kufuatia hatua hiyo ya Baraza la Usalama, Bwana Ban ameeleza kuridhishwa na hatua hiyo na kusema kuwa inadhihirisha azma ya Jumuiya ya kimataifa ya kutokomeza silaha za kemikali.

(Sauti ya Ban)

“Tuna muda mfupi sana lakini Umoja wa Mataifa umejizatiti kushirikiana na OPCW kukamilisha kazi hiyo. Nami pia niko tayari kabisa kusongesha mbele harakati za kisiasa na kibinadamu kwa maslahi ya wananchi wa Syria.”