Watu 42 wanyongwa nchini Iraq kwa kipindi cha siku mbili na wengine 400 zaidi kunyongwa

11 Oktoba 2013

Watu 42 wamenyongwa nchini Iraq  akiwemo mwanamke mmoja kwa kipindi cha siku mbili zilizopita kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa. Watu hao walinyongwa baada ya  kupatikana na makosa ya kuhusika kwenye vitendo vya ugaidi. Jason Nyakundi na taarifa kamili.

 (RIPOTI YA JASON NYAKUNDI)

Kamishina mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Navi Pillay amesema kuwa vitendo hivyo havikuwa tu kinyume na ubinadamu bali ni ukiukaji wa sheria ya kimtaifa. Pillay amesema kuwa imani ya serikali ya Iraq kuwa hukumu ya kifo inaweza kuzuia vitendo vya kigaidi si kweli baada ya kuendela kuongezeka kwa idadi ya vifo vya raia nchini humo. Takiban raia 5740 waliuawa tangu mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu ikiwa ni mara mbili zaidi ya idadi ya watu waliouawa mwaka 2012. Rupert Colville ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu.

(SAUTI YA RUPERT COLVILLE)

 "Kamishina wa haki za binadamu wa umoja wa Mataifa Navi Pillay amesisitiza mara kwa mara baada ya kunyongwa kwa watu wengi mwaka 2012 na mwaka 2013 kuwa mfumo wa haki nchini Iraq una kasoro nyingi. Kunyongwa kwa watu wengi kama huku kumefanyika mara kadha kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita nchini Iraq na si tu  kinyume na ubinadamu bali  ni sawa na ukiukaji wa sheria ya kimataifa. Pia yanahujumu itihada za kujenga taifa lililo dhabiti la Iraq. Kunyongwa kwa watu wengi kulikofanyika siku mbili zizizopita ni ya kipotovu  ikiwa  tu jana ndipo kuliadhimishwa siku ya kupinga hukumu ya kifo duniani."

 Ofisi ya haki za binadamu inasema kuwa zaidi ya watu 348 wamenyongwa nchiniIraqtangu mwaka 2010 huku wengine zaidi ya 400 wakiwa kwenye orodha ya kunyongwa.