Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majanga yanapotokea,walemavu hupata madhara zaidi: Wahlström

Majanga yanapotokea,walemavu hupata madhara zaidi: Wahlström

Mazingira wanayokumbana nayo walemavu wakati wa kukabiliana na majanga bado si nzuri, amesema mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye utekelezaji wa mkakati wa kupunguza athari za majanga Margareta Wahlström katika maadhimisho ya kimataifa ya siku hiyo tarehe 13 mwezi huu inayomulika zaidi walemavu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Wahlström amesema utafiti uliofanyika duniani kuhusu mifumo ya kusaidia walemavu wakati wa majanga umebaini kuwa bado idadi kubwa hukumbwa na majanga zaidi kwani wanapata shida sio tu katika kujiokoa bali pia kupata taarifa kuhusu uwezekano wa kuwepo majanga na mahali pa kuelekea. Amesema utafiti huo hadi sasa umehusisha watu Elfu Sita na bado unaendelea hadi mwisho wa mwaka huu.

(Sauti Margareta)

“Inaonyesha kuwa asilimia 70 ya washiriki wote wamesema hawafahamu mifumo iliyipo, na hatujui kwenye jamii yetu twende wapi. Swali likauliza je unataka kushiriki? Asilimia 50 wamesema ndio, asilimia 25 wamesema hawajui la kusema na kiasi kidogo wamesema hapana. Lakini takwimu muhimu ni hizi za mwisho kufahamu kwa nini mtu anakataa fursa kama hii. Na inaonyesha watu wanategemea zaidi ndugu, jamaa na familia wanaposaka usalama. Lakini pia hata kama kuna mifumo mizuri ya hadhari, mifumo hiyo haizingatii mahitaji maalum ya viziwi, wenye uoni hafifu. Kwa hiyo kuna mambo hayo na unaona hatari kubwa ni kwamba unawaweka walemavu wote katika kundi moja badala ya kutenganisha mahitaji ya kila kundi.”

Mwakilishi huyo maalum wa Katibu Mkuu amesema majanga yanapotokea, idadi ya walemavu wanaopoteza maisha inakuwa ni kubwa na katika maeneo mengine inakuwa maradufu na kwamba hata baada ya majanga, maeneo ya hifadhi ya muda hayazingatii mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu.