Hatma ya watoto wakimbizi wa Syria nchini Jordan mashakani: UNICEF

10 Oktoba 2013

Maelfu ya wakimbizi watoto kutoka Syria walioko nchini Jordan wako hatarini kutelekezwa na hata kutumikishwa, hiyo ni kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.

Inaelezwa kuwa zaidi ya watoto hao 120,000 hawaendi shule ilhali wengine Elfu Thelathini wanatumikishwa katika ajira kama njia mojawapo ya kuwawezesha kukidhi mahitaji yao.

UNICEF inasema ina wasiwasi kuhusu hatma ya watoto hao hususan wa kike nchini Jordan ikisema kuwa idadi ya watoto wa kike wanaolazimishwa na familia zao kuolewa inaongezeka.

Naibu Mwakilishi wa UNICEF nchini Jordan Michele Servadei, anasema hatma ya watoto wa Syria nchini Jordan iko mashakani na kwamba wengi wao wanakabiliwa na msongo wa mawazo kutokana na mambo waliyoshuhudia ikiwemo ghasia na kutumikishwa.

(Sauti ya Michele)

Hivi karibuni tulifanya tathmini ambapo kuna ongezeko kwa asilimia Sita za ndoa za utotoni kati ya mwaka 2001 na 2012. Hofu yetu nyingine ni kwamba kuna ndoa ambazo hazisajiliwi. Hatufahamu ni kwa kiasi gani lakini tunafahamu wako hatarini zaidi kiafya kwa mtoto mdogo wa kike kuolewa, mara nyingi wanaacha shule, lakini wakati huo huo ni hatari zaidi kwa mtoto atakayezaliwa na wanandoa hao. Wakati asilimia 99 ya watoto walioulizwa wamesema wanataka kwenda shule, wazazi hawaoni uharaka wa hilo. Tarkibani asilimia 20 hadi 25 wanasema wanarejea Syria sasa kwa nini waandikishe watoto wao shule. Lengo letu hapa ni kwamba hata kama ni kwa siku chache, inamfanya mtoto ajisikie katika hali ya kawaida na inahakikisha kuwa mtoto anakua katika malezi sahihi na maisha yake ya baadaye yanajengeka.”

Kwa sasa Jordan inahifadhi takribani wakimbizi wa Syria 540,000.