Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi za ASEAN zimesonga mbele kutekeleza malengo ya milenia: Ban

Nchi za ASEAN zimesonga mbele kutekeleza malengo ya milenia: Ban

Umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia, ASEAN umetumia kikao chao cha pamoja kutathmini miaka miwili ya azimio la pamoja kuhusu ubia wao ambapo Katibu Mkuu Ban Ki-Moon amesema nyaraka hiyo imejenga msingi wa ushirikiano ambao unakua na kuimarika kila siku hususan katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia. Grace Kaneiya na ripoti kamili.

(Ripoti ya Grace Kaneiya)

Mjini Darussalam, nchini Brunei ndiko kikao hicho kimefanyika lengo kutathmini azimio hilo la pamoja la Bali. Katibu Mkuu Ban akataja maeneo manne muhimu ambamo kwayo ubia wa Umoja wa Mataifa na ASEAN unaweza kuwa na matokeo ya manufaa kwa pande zote mbili. Maeneo hayo ni muunganiko wa kikanda, maendeleo endelevu, amani na usalama pamoja na haki za binadamu….

(Sauti ya Ban)

“Eneo la ASEAN ni moja ya maeneo duniani yenye tamaduni, imani na mila za kipekee. Amani na maendeleo endelevu kwa wote vyategemea uhusiano na maelewano baina ya jamii na mataifa. Tunapaswa kuepuka tofauti za usawa zinazoibuka na kuleta madhara, toafuti ambazo mara nyingi zinatokana na misingi ya dini na kabila. Umoja wa Mataifa uko tayari kushirikiana nanyi nyote kuendeleza haki za binadamu kwa ajili ya utulivu na maendeleo.”

Kuhusu malengo ya maendeleo ya Milenia, Bwana Ban amepongeza nchi za ASEAN kwa hatua, lakini akasema ushirikiano wahitajika ili kutimiza malengo yote kwa nchi zote na pia katika kuandaa ajenda ya baada ya mwaka 2015 ambapo kutokomeza umaskini ni kipaumbele lakini maendeleo endelevu ni mwongozo na msingi wa kila jambo.