Mienendo ya ukuaji wa kiuchmi yatazamiwa kubadilika: IMF

9 Oktoba 2013

Shirika la Fedha Duniani, IMF limesema kuwa linatarajia uchumi wa kimataifa utakuwa kwa asilimia 2.9, kiwango ambacho ni chini ya asilimia 3.2 ilorekodiwa mwaka 2012.

Katika taarifa yake ya karibuni zaidi kuhusu makadirio ya kiuchumi, IMF inasema ukuaji unatazamiwa kuongozwa na chumi zilizoendelea, huku masoko yanayoibuka yakiwa hafifu zaidi kuliko yalivyotarajiwa.

Olivier Blanchard, ambaye ni Mtaalam Mkuu wa Uchumi wa IMF, ametaja makadirio hayo kama habari nzuri kwa chumi zilizoendelea kama Marekani, Japan na Ulaya, ambako ukuaji umeanza tena, huku akisema ni habari zisizo za kufurahisha kwa chumi zinazoibuka.

(SAUTI YA OLIVIER BLANCHARD)

“Katika nchi nyingi ukuaji umekuwa chini ya vile tulivyotarajia, na umerudi chini kwa miaka miwili ilopita. Kwa mtazamo wa hali nzima duniani, hususan masoko yanayoibuka, kuna athari mbili: Marekani inapozidi kuimarika, ni habari nzuri, lakini viwango vyake vya riba ambavyo huenda vikachangia kutoa fedha nje, huenda isiwe habari nzuri sana. Kwa nchi nyingi, athari hizi zitakuwa nzuri, kwa nyingine, huenda zisiwe nzuri. Hiyo ndiyo hali tunayoitarajia kwa miaka michache ijayo."