Kongomano kuhusu ajira za watoto laanza Brazil

8 Oktoba 2013

Kongamano la tatu la kimataifa kuhusu ajira za watoto limeanza leo kwenye mji mkuu wa Brazil, Brasilia. Kongamano hilo limeandaliwa na serikali ya Brazil, ambayo imezialika nchi zote 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa kushiriki kwa minajili ya kuongeza juhudi za kimataifa za kupinga ajira za watoto. Joshua Mmali na taarifa kamili

(TAARIFA YA JOSHUA)

(Orchestra sounds)

Ndivyo mambo yalivyokuwa kwenye ukumbi wa kongamano hilo la siku tatu, wakati likifunguliwa kwenye mji wa Brasilia, Brazil. Kongamano linatarajiwa kutoa nafasi kwa serikali, wadau wa kijamii na mashirika ya umma kutafakari kuhusu hatua zilizopigwa tangu kongamano la kimataifa lililofanyika mjini The Hague, Uholanzi mnamo mwaka 2010, na kujadili njia za kuongeza juhudi za kimataifa za kupinga ajira za watoto, hususan aina mbaya zaidi ya ajira kama hizo.

Idadi ya watoto wanaoajiriwa kimataifa imepungua kutoka milioni 246 hadi milioni 168 katika muongo mmoja ulopita. Lakini hata ingawa idadi hiyo imepungua, kasi na kiwango cha kushuka huko haitoshelezi kufikia lengo la kutokomeza aina mbaya zaidi za ajira za watoto ifikapo mwaka 2016, kama ilivyokubaliwa na jamii ya kimataifa kupitia kwa Shirika la Kimataifa la Ajira, ILO.

Mkurugenzi Mkuu wa ILO Guy Ryder amesema kuongeza kwa juhudi kunatakiwa ili kuonyesha kuwa kweli kutokomeza kwa baa la ajira za watoto kunatiliwa maanani.