Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM walaani shambulio katika ubalozi wa Urusi nchini Libya.

UM walaani shambulio katika ubalozi wa Urusi nchini Libya.

Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja Mataifa wamelaani vikali shambulio lililoelekezwa kwenye ubalozi wa Urusi mjini Tripoli nchini Libya Oktoba mbili mwaka huu na kusababisha uharibifu ikiwamo majengo.

Wajumbe wameelezea kusikitishwa kwao kuhusiana na shambulio hilo na kusisitiza umuhimu wa kuwafikisha watekelezaji wa shambulio hilo katika vyombo vya sheria. Pia wamesema matendo kama hayo hayakubaliki bila kujali sababu zake na waliotekeleza vitendo hivyo.

Baraza hilo limeitaka Libya kulinda mali za kibalozi na wanadiplomasia na kuheshimu majukumu yao ya kimataifa. Baraza limesisitiza kuheshimiwa kwa mkataba wa Vienna wa mwaka 1961, unaouhusu ulinzi wa mali za kidiplomasia na ule wa mwaka 1963 unaohusu ulinzi wa majengo dhidi ya uharibifu na kuepusha vitendo vya kutowesha amani, kulinda hadhi pamoja na uzuia mashambulizi dhidi ya majengo.