Kuwezesha miji kukabiliana na majanga hakuna mjadala: Ban

4 Oktoba 2013

Katika kuelekea kuadhimisha siku ya makazi duniani, tarehe Saba mwezi huu, shirika la Umoja wa Mataifa la makazi, UN-Habitat limeitisha kikao cha ngazi ya juu kujadili mustakhbali wa makazi hususan mijini ambapo Katibu Mkuu Ban Ki-Moon amesema mabadilio ya tabianchi yanayoshika kasi, kujenga uwezo wa miji kukabiliana na majanga hakuepukiki.

Bwana Ban ametolea mfano wa kimbunga Sandy mwaka mmoja uliopita kilichoacha maelfu huko Caribbean na ukanda wa Mashariki wa Marekani bila makazi,wengine kupoteza maisha na maporomoko ya ardhi huko La Pintada. Amesema majanga hayo ya asili yanaongezeka na tangu kuanza kwa karne hii zaidi ya watu Bilioni Mbili nukta Saba wameathirika na gharama ya kiuchumi ni takribani dola Trilioni Moja nukta Tatu. Amesema mwelekeo wa sasa wa ukuaji miji ni lazima uangaliwe upya…..

“Watendaji wote wafanye kazi pamoja kuokoa maisha, kulinda mali na kuhakikisha huduma zinakuwepo wakati wa majanga. Kuweka mipango ni muhimu. Pindi makazi yanapopanuka kuzingira miji ya zamani, jamii zinaweza kuwa hatarini zaidi. Jibu moja ni kubadili mwenendo wa ukuaji miji. Badala ya kugeuza maeneo ya vilimani na mabonde kuwa  makazi duni , maeneo hayo yaachwe kama yalivyo ili kutoa huduma stahili za kibayonuai kama vile udhibiti wa mafuriko na hata kuepusha maporomoko ya ardhi.”

Bwana Ban ametaka katika siku ya makazi duniani kila mtu ajizatiti kuhakikisha miji inaweza kufikiwa na watu wote, inaweza kukabiliana na majanga na kwamba shughuli za uchumi zinazofanyika zisiwe na madhara kwa mazingira.