Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chagizo lahitajika kupiga marufuku hukumu ya kifo kote duniani: IPU

Chagizo lahitajika kupiga marufuku hukumu ya kifo kote duniani: IPU

Muungano wa Kimataifa wa Wabunge, IPU, umesema ingawa hatua muhimu zimepigwa ama kupiga marufuku hukumu ya kifo au kusitisha utekelezaji wa hukumu hiyo kwa kipindi cha miaka kadhaa, chagizo kubwa zaidi lahitajika kupiga marufuku hukumu hiyo kote duniani. Joshua Mmali na taarifa kamili

(Taarifa ya JOSHUA MMALI)

Katika kuadhimisha Siku ya Kupinga Hukumu ya Kifo Duniani ambayo ni Oktoba 10, Muungano wa Wabunge, IPU na Tume ya Kimataifa ya Kupinga ya Hukumu ya Kifo, ICDP zitaandaa mkutano wa siku moja mjini Geneva, ambao utawaleta pamoja wabunge kutoka kote duniani.

Mkutano huo ambao unawalenga hasa wabunge kutoka nchi ambazo bado zina hukumu ya kifo ingawa huenda zinakusudia kuipiga marufuku, unatarajiwa kuwapa wabunge hao maelezo kuhusu kinachohitajika ili kutokomeza utekelezaji wa hukumu hiyo.

Miongoni mwa vitu vitakavyofanyika ni uendelezaji wa uelewa bora zaidi kuhusu mienendo ya kaimataifa na kikanda kulihusu suala la hukumu ya kifo, pamoja na kutambua nafasi za kisheria na kisiasa zilizopo ili kuwasaidia wabunge kukabiliana na changamoto ambazo nchi nyingi hukumbana nazo katika kupiga marufuku hukumu ya kifo. Wabunge hao watazingatia mifano ya uzoefu wa nchi kama Ufaransa, Kazakhstan na Morocco.