Timu ya kuangamiza silaha za kemikali Syria yaridhishwa na mwanzo wa zoezi

3 Oktoba 2013

Timu ya pamoja ya shirika la kimataifa la kuzuia matumizi ya silaha za kemikali na Umoja wa Mataifa iliyopewa jukumu la kuisadia Syria katika kukomesha silaha za kemikali inasema hatua za mwanzo zinaridhisha kufuatia mkutano wa kwanza baina ya serikali ya Syria lakini uchambuzi zaidi hususani michoro ya kiufundi itahitajika na pia baadhi ya maswali inabidi yajibiwe imesema taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Taarifa hiyo inafafanua kwamba timu hiyo ina matumaini ya kuanza kufanya ukaguzi kwenye maeneo kadhaa na hatimaye kuangamiza vifaa wiki ijayo lakini hilo litategemea matokeo ya makundi ya kiufundi yaliyoanzishwa na ushiriki wa wataalamu wa Syria hapo jana.

Makundi haya yanafanya kazi katika maeneo matatu ambayo ni muhimu katika kukamilisha kazi, uhakika wa taarifa zilizokabidhiwa na serikali ya Syria usalama wa timu ya ukaguzi na maandalizi ya nadharia katika kutekeleza lengo ambapo silaha za kemikali na vifaa zinapaswa kuondolewa ifikapo mwaka 2014.