Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya kupinga vurugu na ukatili yaadhimishwa kwenye UM

Siku ya kupinga vurugu na ukatili yaadhimishwa kwenye UM

Hafla maalum imefanyika mnamo Jumatano, Oktoba 2 kwenye Umoja wa Mataifa, kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya kupinga vurugu na ukatili, ambayo ni siku ya kuzaliwa kwa Mahatma Gandhi. Ungana na Joshua Mmali kwa makala ifuatayo

Muziki

Midundo hii kutoka India, ilisikika hapo jana, tarehe 2 Oktoba, ndani ya ukumbi wa mikutano kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York

Muziki

Ni midundo iloambatana na maadhimisho ya Siku ya Kimaifa ya Kupinga vurugu na ukatili, pamoja na siku ya kuzaliwa kwa hayati Mahatma Gandhi, shujaa wa uhuru wa India, ambaye alieneza ujumbe wa kupigania haki na uhuru bila vurugu au ghasia. Hafla hiyo iliandaliwa na ubalozi wa India kwenye Umoja wa Mataifa, na balozi wa kudumu, Asoke Kumar Mukerji alikuwa na ujumbe huu

Kwa kuwa kunaendeleza mazungumzo na uelewano, kutoandama vurugu kumejitokeza kuwa chombo muhimu cha kisera, iwe ni katika kutatua mizozo ya silaha au kutoa mkakati wa ukuaji na maendeleo, au kama ulimbo unaowaunganisha wanadamu, licha ya tofauti zetu nyingi.”

Mgeni wa heshima, alikuwa ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon

Umoja wa Maatifa unashabikia utatuaji wa mizozo kwa njia ya amani na kukomesha aina zote za ukatili, ziwe za vyombo vya dola au zinazotokana na utamaduni. Tupate nguvu kutoka kwa ujasiri wa watu kama Mahatma Gandhi. Jiepushe na migawanyo na chuki. Chukua msimamo kutetea haki.”

Kama Bwana Ban, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, John William Ashe, alisisitiza haja ya kuandama njia isopendelea vurugu

“Njia ya kupinga vurugu haihusu tu kuubadili ulimwengu, bali pia kumbadili mtu binafsi. Na Mahatma Gandhi alitukumbusha kuwa njia hii ndiyo ya watu jasiri, na sio ya waoga. Tuna jukumu la kutumia vyombo vya kupinga vurugu na ukatili, ili kusaidia kuweka dunia yenye amani kwa wote.

Wawakilishi wa nchi mbali mbali walitoa hotuba za kumuenzi Mahatma Gandhi na wengine kama Martin Luther King Jr na Nelson Mandela, na kusisitiza haja ya kuepuka vurugu, kuvumiliana na kuendeleza mazungumzo ya amani. Pamoja na hayo, muziki zaidi, hasa ule, aloupenda saana Mahatma Gandhi.

Muziki