Ajira zisizo rasmi zitambulike ili kuondoa tatizo la wahamiaji wasio na vibali: Mtaalamu

3 Oktoba 2013

Kila wakati tunasikia wahamiaji wasio na vibali, vipi kuhusu waajiri wanaokiuka sheria ? Amehoji Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za wahamiaji, François Crépeau katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu mjadala wa ngazi ya juu unaongalia uhamiaji na maendeleo. Amesema penye wahamiaji wasio na vibali kuna waajiri wanaowapatia ajira kwenye nyanja ambazo ni muhimu kwa uchumi wa nchi lakini mamlaka hazitaki kutambua ajira hizo na hata wahamiaji hao.

(Sauti ya Crépeau)

“Kila wakati tunazungumzia wahamiaji wasio na vibali au wafanyakazi wahamiaji wasio na vibali, lakini kamwe hatuzungumzii waajiri wanaokiuka sheria. Nchi zina mahitaji ya ajira yasiyotambuliwa ambayo huwa katu hatujadili. Kile kinachoitwa ajira za ujuzi wa chini kama kwenye sekta ya kilimo, ujenzi, hospitality na kazi za majumbani, na hatutaki kutambua hilo na sababu mojawapo ni kwamba iwapo tutazitambua, watu wataanza kudai haki zao, kima cha chini cha mshahara na hilo litaongeza gharama kwenye sekta hiyo ambayo inaonekana ina faida ndogo ya kiuchumi.”

Kuhusu janga la kuzama boti huko Lampedusa, mtaalamu huyo amesema misafara ya wahamiaji haijaanza leo bali tangu zamani na haikuwa na majanga kama wakati huu kwani hivi sasa nchi zinaona kuvuka mpaka ni kosa la jinai na ametoa pendekezo..

(Sauti ya Crépeau)

Kutatua suala la uhamiaji haramu kwa njia kandamizi pekee, matokeo yake ni kile tulichohudia Lampedusa. Nafikiri njia mojawapo ambayo Umoja wa Ulaya inaweza au inapaswa kufanya kutatua hali hiyo ni kuwawezsha wahamiaji ikiwemo wale wasio na vibali kudai haki zao, na hilo si jambo ambalo linawezekana kirahisi.”