Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban apongeza hatua ya Baraza la Usalama kuhusu usaidizi wa kibinadamu Syria

Ban apongeza hatua ya Baraza la Usalama kuhusu usaidizi wa kibinadamu Syria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amekaribisha taarifa ya Rais wa Baraza la Usalama iliyotolewa leo na kuridhiwa na wajumbe wa baraza hilo ambayo inalenga kushughulikia hali mbaya ya kibinadamu nchini Syria na kuonyesha azma ya jumuiya ya kimataifa ya kusaidia wananchi wa Syria kuondokana na mzozo unaoendelea kuwakumba. Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemkariri Bwana Ban akisema kuwa iwapo kilichomo kwenye taarifa hiyo kitatekelezwa kwa dhati na kwa hatua zilizobainishwa, basi wafanyakazi wanaotoa msaada wataweza kuwafikia mamilioni ya wasyria ambao sasa wako kwenye hali ya sintofahamu kwa miezi kadhaa sasa kuhusu jinsi ya kupata mahitaji muhimu. Bwana Ban pia amerejelea wito wa Baraza la Usalama kwenye taarifa hiyo unaotaka pande zote husika nchiniSyriakuwezesha utoaji huo wa misaada ya kibinadamu na kukumbusha kuwa yeyote anayekiuka haki za kimataifa za usaidizi wa kibinadammu na haki za binadamu atawajibika.