Mkataba wa kupinga uhalifu wa kupangwa waadhimisha miaka 10

2 Oktoba 2013

Uhalifu wa kimataifa wa kupangwa ni biashara kubwa ambayo faida yake inakadiriwa kuwa dola bilioni 870 kila mwaka, huku ukiathiri idadi isojulikana ya watu. Miaka kumi ilopita, mkakati wa kwanza wa kuupiga vita uhalifu huo ulianza kutekelezwa, kupitia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kupinga Uhalifu wa Kimataifa wa Kupangwa, kama hatua ya kujitoa kwa jamii ya kimataifa kukabiliana na changamoto hiyo sugu.

Uhalifu wa kimataifa wa kupangwa hujumuisha uhalifu wote unaochochewa na hamu ya kupata faida, na hutekelezwa na makundi kutoka zaidi ya nchi moja. Ili kutoa mafunzo na kueleza uhalifu huu kwa jamii ya kimataifa, Ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Madawa na Uhalifu ilizindua kampeni kuhusu uhalifu wa kimataifa wa kupangwa mnamo mwaka 2012, ambayo ilijumuisha maelezo ya video kuhusu aina tofauti za uhalifu huo, pamoja na gharama yake ya kibinadamu na kifedha.

Miongoni mwa vitendo ambavyo vinaweza kutajwa kuwa sehemu ya uhalifu wa kimataifa wa kupangwa ni ulanguzi wa madawa ya kulevya, uvushaji wa magendo wa wahamiaji, usafirishaji haramu wa watu, ulanguzi wa fedha, usafirishaji haramu wa silaha, wanyama wa pori na bidhaa za kitamaduni. Kila mwaka, idadi ya watu isojulikana hupoteza maisha yao kutokana na uhalifu huu wa kupangwa.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter