UNICEF yasikitishwa na mauaji ya watoto 12 Syria

1 Oktoba 2013

Shirika la Kuhudumia Watoto katika Umoja wa Mataifa, UNICEF, limesikitishwa na kuripotiwa kwa vifo vya watoto 12 katika shambulizi la angani dhidi ya shule moja ya sekondari eneo la Ragga, kaskazini mashariki mwa Syria, mnamo tarehe 29 Septemba.

Ripoti kutoka eneo la tukio zinasema watu 14 – wengi wao wanafunzi- waliuawa katika shambulizi hilo dhidi ya shule ya kibiashara ya Ibn Tufail mwendo wa saa mbili asubuhi, siku ya kwanza ya mwaka mpya wa shule.

UNCEF imesema vitendo kama hivyo vinaonyesha hatari wanazokumbana nazo watoto wakati wa mzozo uliopo nchini Syria sasa, na pia vinasaidia kueleza ni kwa nini wazazi wengi hawataki kuwapeleka watoto wao shule. UNICEF imelaani vikali shambulizi hilo na kutoa tena wito kwa pande zote katika mzozo wa Syria kukoma kulenga shule na kuzitambua kama maeneo ya amani ambako watoto wanaweza kupata msaada.