Timu ya OPCW na ya UM yawasili Damascus na kuweka kituo:

1 Oktoba 2013

Timu ya pamoja ya Umoja wa Mataifa na ya kupinga matumizi ya silaha za kemikali OPCW, imewasili nchini humo siku nne baada ya baraza la utendaji la OPCW na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha bila kupingwa mipango ya kutuma timu hiyo Syria kuanza mchakato wa kusimamia kazi ya kuharibu mipango ya silaha za kemikali ya nchi hiyo.

Timu hiyo ambayo inajumuisha wakaguzi 19 wa OPCW na wafanyakazi 14 wa Umoja wa Mataifa imekwenda Syria kwa njia ya barabara kutoka Beirut Lebanon bila kupata adha yoyote.Serikali ya Syria ilitoa kibali cha kusafiria Viza na kuwawezesha kufika Damascus.

Ilipowasili timu ya pamoja ya OPCW na Umoja wa Mataifa ilianzisha kituo cha masuala ya logistiki kwa ajili ya kuanza kazi mara moja.

Katika siku zijazo juhudi zao zinatarajiwa kujielekeza kuthibitisha taarifa zilizotolewa na serikali ya Syria na mipango ya awali ya kuisaidia nchi hiyo kusambaratisha vituo vyake vya uzalishaji wa silaha zake za kemikali. Baraza la OPCW na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wameamua zoezi hilo likamilike ifikapo Novemba Mosi mwaka huu.

Kwa mujibu muda wa mwisho wa OPCW na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa silaha zote za kemikali lazima ziwe zimetokomezwa katika nusu ya kwanza ya mwaka ujao.