Ban na Waziri Amina wazungumzia Somalia, ICC na wakimbizi

1 Oktoba 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amekuwa na mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Bi. Amina Mohammed mjiniNew York, ambapo kwa mara nyingine tena Ban ametuma salamu za rambirambi kwa serikali na wananchi kufuatia shambulio la mwezi uliopita huko Nairobi. Amesema Umoja wa Mataifa uko tayari kutoa usaidizi kwa kadri ya  uwezo wake huku akiishukuru Kenya kwa mchango wake wa kuleta utulivu huko Somalia. Bwana Ban pia amekaribisha mpango wa utatu kati ya serikali ya Kenya, Somalia na shirika la wakimbizi duniani UNHCR la kushirikiana kuwezesha mpango wa kurejesha nyumbani kwa hiari wakimbizi waSomalia.  Katibu Mkuu pia ameisihi Kenya iendelee kutoa ushirikiano kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC.