Mpango wa kwanza wa kutokomeza vifo vya TB kwa watoto waainishwa:WHO

1 Oktoba 2013

Mpango wa kwanza unaoainisha hatua za kuchukuliwa kutokomeza vifo vitokanavyo na kifua kikuu umezinduliwa Jumanne nchini Marekani limesema shirika la afya duniani WHO. Flora Nducha na taarifa kamili

(RIPOTI YA FLORA NDUCHA)

Vifo zaidi ya 74,000 vya watoto vitokanavyo na kifua kikuu vinaweza kuzuilika kila mwaka kupitia hatua zilizoainishwa katika mpango huo wa kwanza maalumu kwa ajili ya watoto na kifua kikuu. Mpango huo “njia kwa ajili ya Tb ya watoto: kuelekea vifo sufuri, umezinduliwa na wadau wa kimataifa wa kupambana na kifua kikuu mjini Washington DC na kukadiria kwamba dola milioni 120 kwa mwaka zitasaidia saana kuokoa maisha ya maelfu ya watoto kutoka kwa maradhi ya kifua kikuu wakiwemo watoto ambao tayari wameathirika na Tb na HIV. Kila siku zaidi ya watoto 200 wa chini ya umri wa miaka 15 wanakufa kutokana na kifua kikuu , ugonjwa ambao unazuilika na kutibika. WHO inakadiria kwamba kisa kimoja kati ya 10 vya kifua kikuu kimataifa ni vya watoto wa umri huo na idadi inaweza kuwa kubwa kwa kuwa watoto wengi hawapimwi.