Wazee wana haki ya kuishi maisha yenye staha: Ban

1 Oktoba 2013

Katika kuadhimisha siku ya wazee duniani hii leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametaka serikali kujizatiti kuondoa vikwazo vyote vinavyowanyima wazee haki zao za msingi na kuwafanya waishi maisha yasiyo na staha.

Ujumbe wa Bwana Ban unaeleza bayana kuwa idadi kubwa ya wazee wanaishi maisha dhalili katika jamii zao wakihaha kupata huduma za msingi kama vile chakula, malazi, kujisafi na hata maji safi na salama.

Amesema ni kutokana na hilo katika ripoti yake ya mwelekeo baada ya mwaka 2015 ametaka mambo hayo yazingatiwe ili dunia iwe na fursa ya maisha ya staha kwa makundi yote.

Bwana Ban amesema mwelekeo wa dunia hivi sasa ni mabadiliko ya mjumuisho wa makundi ambapo ifikapo mwaka 2050 idadi ya wazee itakuwa maradufu ya idadi ya watoto katika nchi zilizoendelea huku katika nchi zinazoendelea idadi ya wazee itakuwa maradufu.

Hivyo amesema mabadiliko hayo yatakuwa ni fursa na changamoto kwa nchi husika, akitanabaisha kuwa ni fursa kwani ni wakati wa kutumia busara na uwezo wa wazee na ni changamoto kwa kuwa ni vyema kupitisha sera ambazo zitaweka mtangamano na mshikamano katika jamii.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter