Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu waingia siku ya sita

30 Septemba 2013

Mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umeingia siku yake ya sita hii leo, kwa hotuba kutoka kwa wawakilishi wa nchi tofauti. Wa kwanza kuzungumza hii leo ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada, aliyeanza hotuba yake kwa kuwaenzi wahanga wa ugaidi. Joshua Mmali ana taarifa zaidi

(TAARIFA YA JOSHUA)

Katika hotuba yake kwenye Baraza Kuu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada John Baird amesema kuwa uhalifu wa ugaidi ni tatizo kwa ubinadamu mzima, na kila unapotendeka, familia ya ubinadamu ni moja katika uchungu, katika uombolezaji na katika kupiga moyo konde na kusema uovu hautashinda.

"Ningependa kuwaenzi wahanga wa ugaidi. Nawaenzi wahanga wote popote pale, wakiwemo wale walouawa katika shambulizi la Westgate mjini Nairobi. Tuliwapoteza raia wawili wa Canada, akiwemo mwanadiplomasia mjini Nairobi. Wakati huu wa huzuni, umoja wa ubinadamu ndio kauli mbiu yangu. Hapa kwenye Umoja wa Mataifa, Canada inajikita katika masuala ya usalama na matokeo ya kuifana familia ya ubinadamu."

Waziri huyo wa Canada amesema mabilioni ya watu wenye njaa duniani, au wasio na maji safi, au wakimbizi hawajali ni wanachama wangapi wanaoketi kwenye Baraza la Usalama, ila msaada watakaopata kutoka kwa wanadamu wenzao.

Naye Naibu Waziri Mkuu wa Syria Walid al-Moualemameangazia suala la usalama katika hotuba yake, akisema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, hali imezidi kuwa ya kuyumbayumba kote duniani. Kuhusu taifa lake, amesema makundi ya kigaidi yakiwemo Al Qaeda yameshaingia katika mzozo uliopo na kutekeleza vitendo vya kikatili.

"Kinachotendeka nchini mwangu ni dhahiri kwa kila mmoja, lakini baadhi ya nchi hazitaki kutambua kuwa Al qaeda, kundi hatari zaidi la kigaidi na wafuasi wake wanapigana nchini Syria. Katika nchi yangu Bwana Rais, vichwa vya watu wasio na hatia vinaangikwa kwenye vijiti kwa sababu tu eti hawaungi mkono misimamo mikali ya al qaeda"

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud