Taaluma ya ualimu iheshimiwe, elimu ya leo itoe fursa ya ajira kesho: ILO

30 Septemba 2013

Hadhi ya walimu lazima ilindwe na wasomi wenye vipaji washawishiwe kuchukua taaluma ya ualimu, ni kauli ya Mkurugenzi mkuu wa Shirika la kazi duniani, ILO Guy Ryder kwa siku ya walimu duniani tarehe Tano mwezi Oktoba kama anavyoripoti Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Mkuu huyo wa ILO amesema walimu wanapaswa kupatiwa mazingira bora ya kazi na jukumu lao la kutoa haki ya msingi ya elimu lisiwe linatumbukia kwenye mtego wa bana matumizi ya serikali. Amesema ni wajibu wa serikali, vyama vya wafanyakazi na taasisi za kiraia kuchukua hatua kulinda hilo huku zikishawishi wananchi wenye vipaji kujiunga na kada hiyo..

(sauti ya Guy)

“Hadhi ya taaluma ya ualimu lazima iheshimiwe kupitia mazingira bora ya kazi ikiwemo kuwa huru kujiunga na vyama vyao na fursa ya kuandaa sera za elimu.”

Ryder akaenda mbali zaidi na kusema kuwa elimu bora ni lazima itoe fursa ya mwanafuzi kupata ajira katika zama za sasa za uchumi wenye ushindani.

(Sauti ya Rider)

“Na hilo linataka ushiriki thabiti wa sekta binafsi, na vyama vya wafanyakazi na sera bora ya elimu ili kuhakikisha kuwa elimu ya leo inatoa fursa ya ajira kesho.”