Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Quartet yakutana kuzungumzia hatua za majadiliano baina ya Israel na Palestina:

Quartet yakutana kuzungumzia hatua za majadiliano baina ya Israel na Palestina:

Wawakilishi wa Quartet ambao ni Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon, waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov, waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry, na mwakilishi wa sera za nje na usalama wa Muungano wa Ulaya Catherine Ashton,wamekutana mjini New York leo kando na mjadala wa baraza kuu .

Katika mkutano wao aliongezeka pia mwakilishi wa Quartet Tony Blair, mpatanishi mkuu wa Israel ambaye pia ni waziri wa haki na sheria Tzipi Livni na mpatanishi mkuu wa Palestina Saeb Erekat. Waziri Kerry ameifahamisha Quartet kuhusu hatua zilizopigwa katika majadiliano baina ya Israel na Palestina tangu kuanza kwa mazungumzo 29 Julai mwaka huu.

Quartet imerejea kusisitiza nia yake ya kutoa msaada katika pande zote katika juhudi za kupata suluhu ya ya makubaliano ya kudumu katika muada wa miezi 9 ulioafikiwa. Nia ni kupata suluhu ya kudumu katika mzozo baina ya majirani hao wawili.

Quartet imepongeza juhudi za uongozi wa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas kwa kuendelea kujihusisha na majadiliano ili kushughulikia masuala muhimu.

Quartet imezitaka pande zote kuchukua kila hatua inayowezekana kuchagiza mazingira mazuri ya kuleta mafanikio ya mchakato wa majadiliano na kujizuia na hatua zozote zitakazotia dosari na kuvunja imani ya kufikia hatima ya suala hilo.

Wajumbe wa Quartet wamesema wataendelea kuwasiliana kwa karibu na pande hizo mbili kuhakikisha zinapata msaada unaohitajika katika majadiliano.