Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mawaziri wa muungano wa ustaarabu wakutana kuridhia mkakati mpya wa ushirikiano

Mawaziri wa muungano wa ustaarabu wakutana kuridhia mkakati mpya wa ushirikiano

Hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, mkutano wa mawaziri wa nchi marafiki wa Muungano wa Ustaarabu, UNAOC, umefanyika pembezoni mwa mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo.Alice Kariuki ana maelezo zaidi

(TAARIFA ya ALICE)

Mbali na kupokea maelezo zaidi kuhusu maandalizi ya mkutano ujao wa kimataifa wa muungano huo nchini Indonesia, mkutano huo pia umeridhia azimio kuhusu mkakati wa muungano huo wa ustaarabu. Akiongea wakati wa mkutano huo, rais wa muungano huo, Nassir Abdulaziz al Nasser, amesema tunaishi katika ulimwengu mdogo zaidi kuliko zamani kwa sababu ya teknolojia, kwani teknolojia inatusaidia kuwasiliana zaidi.

"Hakuna wakati mwingine katika historia ya mwanadamu, ambako tumekuwa na uwezo wa kufahamu zaidi kuwahusu wale walio tofauti na sisi. Kuweza kuwafikia na kupata habari kuhusu wengine, kunaweza kuwa njia nzuri ya kuunganisha wanadamu. Lakini pia, njia hiyo pia inaweza kutumiwa kwa njia ya kutenganisha na uharibifu. Mawazo hayana tena mipaka. Teknolojia ya mawasiliano na habari imezifanya kuwa na sura ya kimataifa."

Bwana al Nasser amesema katika ulimwengu wa sasa, upatikanaji wa habari ni sehemu muhimu ya maisha, na unaweza kuchangia maendeleo, au ukitumiwa vibaya, unaweza kuleta migogoro na migawanyo.