Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Arobaini ya Al Shabaab kutimia, ICC yatia mashaka:Rais Mohamoud

Arobaini ya Al Shabaab kutimia, ICC yatia mashaka:Rais Mohamoud

Rais Hassan Sheikh Mohamoud wa Somalia ameliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa uthabiti wa kikundi cha kigaidi nchini Somalia unazidi kuzorota lakini bado jitihada zaidi za kimataifa, kikanda na kitaifa zinahitajika ili kuweza kusambaratisha kabisa kikundi hicho kinachoendelea kuua raia wasio na hatia. Amesema tukio la Kenya hivi karibuni kinadhihirisha kuwa jitihada zaidi za pamoja zahitajika ikiwemo usaidizi wa kifedha kwa taasisi za usalama kwani kwa sasa nchini Somalia wameweza kukishinda kijeshi na kinachotakiwa ni kukabiliana na itikadi isiyo sahihi wanayoipandikiza pembe ya Afrika kupitia mitandao ya kijamii, vyombo vya habari na hata kwenye shule na vyuo vikuu. Baada ya hotuba hiyo, Rais Mohamoud katika mahojiano na Assumpta Massoi wa Radio ya Umoja wa Mataifa ametaja sababu za ushawishi wa Al Shabaab.

(Sauti ya Rais Mohamoud)

“Idadi kubwa ya wapiganaji wa Al Shabaab hawapigani kwa misingi ya itikadi, bali kuna mambo mengine kama vile umaskini, ukosefu wa fursa za ajira, na wananchi wengi hawajaenda shule kwa zaidi ya miaka 20, mambo haya yakiwekwa pamoja yanasababisha hali hiyo. Iwapo tukiwapatia njia mbadala ya maisha kwa vijana, fursa za ajira, elimu na waweze kukidhi mahitaji yao endelevu, basi nafikiri Al Shabaab inaweza kushindwa.”

Wakati Afrika inachagiza hoja ya kwamba mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC inatizama zaidi upande mmoja hususan Afrika na kufumbia macho matukio mengine ya uhalifu kwenye maeneo mengine, nilimuuliza Rais Mohamoud msimamo wake, na alisema….

(Sauti ya Rais Mohamoud)

“Vile inavyoshughulikia mambo hivi sasa siyo sahihi. Hii si mahakama kwa viongozi wa Afrika. Kuna mizozo, lakini pindi suluhisho linaanza kupatikana na maridhiano yanaanza, hapo ndio ICC inakuja, na inakuwa kikwazo cha maridhiano yanayoweza kupatikana kwenye nchi husika. Angalia nchini Kenya, jamii husika zimekubaliana kusonga mbele, na viongozi wao wanapelekwa ICC. Hii italeta shuku na kutokuaminiana baina ya jamii husika. Kwa sasa haisaidii hivyo nafikiri itakuwa vyema ICC ikaangalia upya jinsi ya kushughulikia suala hilo.”