Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujangili wa wanyamapori ni tishio kwa amani na usalama barani Afrika: Rais Bongo

Ujangili wa wanyamapori ni tishio kwa amani na usalama barani Afrika: Rais Bongo

Suala la ujangili wa ndovu na kifaru pamoja na uvunaji haramu wa mazao ya misitu limeangaziwa ndani ya Umoja wa Mataifa hii leo wakati wa kikao cha ngazi ya juu kilichoandaliwa na serikali ya Ujerumani na Gabon. Kubwa lililoibuka ni kutaka Umoja wa Mataifa kuwa na dhima kuu katika kudhibiti matukio hayo kama vile kuwepo kwa mjumbe maalum pamoja na azimio la kudhibiti ujangili wa wanyamapori na uvunaji haramu wa misitu. Rais Ali Bongo Ondimba wa Gabon akasema kuwa biashara hiyo haramu sasa ina thamani ya zaidi ya dola Bilioni 25 kwa mwaka na kutokana na thamani hiyo imevutia wafanyabiashara wakubwa wanaotumia mbinu za kisasa. Amesema askari wanyamapori sasa wanatumia zana kama vile wako uwanja wa vita. Hata hivyo amesema changamoto ni vitendea kazi na janga hilo si la kitaifa tu bali ni la dunia nzima.

(Sauti ya Rais Ali Bongo Ondimba)

“Hapa ningependa kutoa wito wa kuwepo kwa juhudi za pamoja za jumuiya ya kimataifa kushughulikia suala hili, kuanzia vyanzo, mahali bidhaa zinakopitia na nchi ambazo ni masoko, vyote vyapaswa kufanya kazi pamoja. Kwa niaba ya Ujerumani na Gabon namsihi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kumteua mjumbe maalum kuhusu uhalifu wa wanyamapori ambaye atawajibika kuchochea jitihada dhidi ya suala hili muhimu. Tunaona umoja wa mataifa unapaswa kuwa na jukumu la uongozi."