Zimbabwe haitakuwa koloni tena, vikwazo viondolewe: Mugabe

26 Septemba 2013

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amehutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo amegusia masuala ya marekebisho ya muungo wa Umoja wa Mataifa ikiwemo baraza la usalama pamoja na kile alichokiita ni njama za kurejesha ukoloni mamboleno nchini mwake. Rais Mugabe amesema hoja ya Afrika ya kutaka muundo wa Baraza la usalama ufanyiwe na marekebisho ili uwe na uwakilishi sahihi imechukua muda mrefu bila mafanikio na kwamba kuna wakati maamuzi yake yanakuwa ni ya mashaka na hivyo kukwamisha lengo mahsusi la kuanzishwa Umoja wa Matafa la kulinda amani.

(Sauti ya Rais Mugabe)

“Matukio ya hivi karibuni yamedhihirisha kuwa maamuzi ya baraza la usalama yamekuwa yakisitiri vitendo vya nguvu za ukoloni mamboleo zinazotaka kuingilia kijeshi nchi ndogo kwa lengo la kubadilisha serikali na hatimaye kuweza kudhibiti utajiri wao.”

Kuhusu vikwazo dhidi ya nchi yake amesema kuwa havina msingi wowote na kama vilikuwa ni njama ya kufanya mabadiliko ya uongozi basi vimeshindwa kwani wananchi wamezungumza.

(Sauti ya Mugabe)

“Zimbawe ni kwa wazimbabwe na hivyo ndivyo kwa rasilimali zake. Tafadhali hizi nchi ziondoe vikwazo vyao visivyo halali dhidi ya nchi yangu yenye amani. Iwapo vikwazo hivyo vililenga kubadili serikali, matokeo ya uchaguzi wa kitaifa hivi karibu yameonyesha kuwa hawawezi kufanikiwa ajenda yao ya kubadili serikali.”