Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malawi iko mbioni kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia:Banda

Malawi iko mbioni kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia:Banda

Rais wa Malawi Bi Joyce Banda ameliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa nchi yake imepata mafanikio makubwa kwenye nyanja mbali mbali tangu achukue madaraka mwaka 2012. Alice Kariuki na taarifa kamili:

(RIPOTI YA ALICE KARIUKI)

Katika ujumbe wake Bi Banda amesema kuwa kutokana na utekelezaji wa mipango mipya ya kushughulikia changamoto za kisiasa na kiuchumi Malawi uchumi wa nchi umekuwa na kuongezeka hadi asilimia 5 mwaka huu kutoka asilimia 1.8 mwaka jana. Ameongeza kuwa watu wa Malawi kwa mara nyingine tena wanafurahia uhuru wao kama ilivoywekwa katika katiba ya nchi. Kuhusu Malengo ya Maendeleo ya Milenia amesema Malawi imo njiani kufikia manne kati ya malengo hayo lakini bado kuna changamoto kufikia mengine ikwemo kupunguza vifo vya wakina mama wajawazito.

Akizungumza na Joshua Mmali wa idhaa hii baada ya kutoa ujumbe wake, Bi Banda amesema Malawi imeshindwa kufikia malengo ya maendeleo ya milenia kwa sababu ya utawala mbaya:

Kinachonitia hasira sana ni kwamba kulikuwa na uwezo wa kufikia mengi ya malengo ya milenia – hata hivyo najua sasa tutaweza kufikia karibu malengo yote kwa sababu ya utashi wa kisiasa. Kiongozi na uongozi ni muhimu, dhamira yake ndio inayoleta mafanikio.

Akizungumzia jukumu la wanawake katika uongozi Bi Banda ameiambia Radio ya Umoja wa Mataifa kuwa:

Kwa maoni yangu bara la Afrika limeendealea sana kwa sababu baadhi ya mabara bado hayajaweza kuwa na mwanamke kiongozi, ikiwemo nchi ya Marekani. Afrika ina viongozi wawili wanwake na tunaweza kupata wengine. Umoja wa Afrika unaongozwa na mwanamke, sasa kiongozi wa SADC ni mwanamke, Katibu Mtendaji pia ni mwawamke. Jaji Mkuu wa Malawi ni mwanamke, na pia mkuu wa utumishi wa umma, hivyo sisi tunashiriki ipasavyo.

Hata hivyo Bi Banda amesema ni muhimu kupongeza wanaume ambao pia wametoa nafasi ili wanawake waweze kushiriki katika uongozi na kufanya kazi bega kwa bega na wanaume kwa ajili ya kuleta maendeleo katika bara la Afrika.