Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanachama wa UM waridhia azimio la kukabiliana na ubakaji katika vita

Wanachama wa UM waridhia azimio la kukabiliana na ubakaji katika vita

Ubakaji katika vita hautakubalika kuendelea tena. Hayo yamesemwa na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kingono katika maeneo ya vita, Bi Zainab Hawa Bangura, kufuatia kupitishwa kwa azimio la kupinga uhalifu huo wa kivita kwenye hafla maalum kando ya mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Bi Bangura amesema kupitishwa azimio la ahadi za kutokomeza ukatili wa kingono katika vita, na kuzindua mtandao wa mashujaa wa kupinga uhalifu huo, kunampa matumaini makubwa ya kueneza ujumbe kwamba ni wakati wa kuchukua hatua na kutokomeza ubakaji katika vita.

Kuwepo kwenu hapa ni ujumbe kwa watu walio hatarini kote duniani kuwa jamii ya kimataifa, wakati miili yao ikitumiwa kama uwanja wa vita, kwa manufaa ya kijeshi na kisiasa. Siku ambazo ukatili wa kingono katika vita ulipuuzwa kama matukio ya bahati mbaya yatokanayo na vita zimepita. Kwa kuwa sasa tumebadili mitazamo yetu, ni lazima pia tubadili vitendo ili kuzuia na kutokomeza uhalifu huu.

Hafla hiyo imesimamiwa na Bi Bangura, akishirikiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, William Hague, ambaye amesema desturi ya kutowawajibisha wanaoutekeleza ubakaji katika vita, ni mojawapo ya mifano ya kuwanyima watu haki katika historia.

Bwana Hague amesema nchi 106 zimeridhia azimio hilo mpya, ambayo ni ishara ya hatua kubwa ya kihistoria katika uelewa wa kimataifa wa ubakaji na ukatili wa kingono katika vita, na nia ya serikali kukabiliana nao kama suala la kipaumbele.

"Kwanza tumekubaliana kuwa ubakaji na ukatili wa kingono katika vita unakiuka mikataba ya Geneva, aya ya kwanza. Hii inamaanisha washukiwa wanaweza kukabiliwa popote walipo duniani. Pili tumekubaliana kutoruhusu msamaha kwa makosa ya uhalifu katika mikataba ya amani, ili uhalifu huu usifutiliwe mbali. Tatu tumekubaliana kubuni mfumo mpya wa kimataifa mwaka 2014 utakaowezesha ushahidi unaokusanywa kuwa wa kuaminika mahakamani, ili manusura wengi zaidi wapate haki. Nne tumeahidi kuunga mkono na kulinda mashirika ya umma, yakiwemo makundi ya wanawake na wanaharakati wa haki za binadamu, na kuwawezesha waathirika kupata haki."

Msichana Philemona, amehudhuria hafla hiyo, kama mwakilishi wa manusura wa ukatili wa kingono.

"Ningependa mjue hatua hii inachomaanisha kwa yeyote ambaye ameathiriwa na ukatili wa kingono, moja kwa moja au kwa njia nyingine. Kuona kuwa nchi nyingi wanachama zilizopo hapa, ambazo natumai zitasimama bega kwa bega na manusura katika vita vya kutokomeza ukatili wa kingono, hilo linatia kila mmoja moyo, kuendelea kuchukua hatua kutokomeza uhalifu huu."