Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Soko, umaskini na tamaa vichocheo vya ujangili wa ndovu Tanzania

Soko, umaskini na tamaa vichocheo vya ujangili wa ndovu Tanzania

Tanzania imesema ongezeko la bei ya pembe za ndovu huko Mashariki ya Mbali, umaskini wa wananchi na tamaa ya baadhi ya watu ni baadhi ya vichocheo vikubwa kwa ujangili wa tembo nchini humo. Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki amesema hayo katika mahojiano maalum na Idhaa hii mjini New York, Marekani ambako yuko kwa ajili ya kushiriki mkutano wa ngazi ya juu ya nchi za Afrika na Umoja wa Mataifa kuhusu udhibiti wa ujangili wa ndovu.  Amesema mambo hayo yalifanya hali ya ujangili wa tembo kuwa mbaya lakini kwa miezi minane iliyopita hali imeanza kuimarika kutokana na hatua zinazochukuliwa za kuthibiti vitendo hivyo na hata kukamatwa kwa baadhi ya shehena za meno ya ndovu.

(Sauti ya Kagasheki)

Balozi Kagasheki amesema kinachofanyika sasa ni kuimarisha hatua za udhibiti ili kuondokana na kukamata shehena hizo pekee na badala yake kuzuia kabisa ujangili wa tembo na tayari mazungumzo ya hivi karibuni kati ya Rais Jakaya Kikwete na ujumbe wa Marekani huko Washington DC yalikuwa mazuri kwani kuna miradi itakayofadhiliwa na Marekani.

(Sauti ya Kagasheki)