UNHCR yalaani ongezeko la mashambulizi Iraq

24 Septemba 2013

Huko nchini Iraq Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na wakimbizi UNHCR limesema kuwa linatilia shaka kutonana na ongezeko la mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ambayo yamesababisha idadi kubwa ya watu kukosa makazi.

Kumekuwa na mfululizo wa matukio ya mashambulizi ya mabomu na maguruneti hali ambayo imezusha hali ya wasiwasi mkubwa kwa wananchi. George Njogopa na taarifa zaidi

(Taarifa ya George Njogopa)

Zaidi ya raia wa Iraq 5,000 wanaripotiwa kukimbia makazi yao katika kipindi cha kuanzia mwaka huu kutokana na wimbi kubwa la matukio ya mashambulizi ya mambo ya maguruneti. Wengi ya raia hao ni kutoka mji mkuu wa Baghdad ambao wamelazimika kukimbilia katika miji ya Anbar na Salah Al Din huku wengine wakisalia bila makazi katika majimbo ya Diyala na Ninewa. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la UNHCR likishirikiana na wahisani wengine limeanza kuendesha tathmini kwa ajili ya kubaini idadi ya watu waliokosa makazi ili kuwasambazia huduma muhimu.

Baadhi ya huduma hizo ni pamoja na msaada wa vyakula, mahitaji ya elimu, na mahitaji mengine ya kiustawi wa binadamu.

Melissa Fleming ni msemaji wa UNHCR

" Hatua hii ya karibuni imeongeza idadi ya watu waliokosa makazi hadi kufikia milioni 1.13 walioko  ndani ya Iraq kwenyewe  ambao walikimbia mapigano katika kipindi cha tangu mwaka 2006 hadi 2008. Wengi wa raia hao ni wakazi wa miji ya Baghdad, Diyala na Ninewa.

Kiasi cha raia 467,000 wamerejea na kukusanyika katika makazi ya hali ya chini wakiwa kwenye maeneo ya wazi na wengine kwenye nyumba za hali ya chini zinazomilikiwa na serikali, huku wakiwa katika hali ngumu kutokana na kukosa huduma muhimu kama ukosefu wa umeme, kutokuwepo kwa vyanzo mbadala vya maji, ukosefu wa shule na kukosa fursa za ajira”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter