Waloshambulia kambi ya Asharaf Iraq ni lazima wawajibishwe kisheria:UM

24 Septemba 2013

Ofisi ya haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa imeiomba tena serikali ya Iraq kufanya kila iwezalo ili kuwatambua na kuwawajibisha kisheria waliotekeleza shambulizi dhidi ya kambi ya Ashraf, ambako watu 52 waliuawa.

Mnamo Septemba 3, ofisi hiyo ilitoa taarifa ya kulaani shambulizi hilo, na kutoa wito kwa serikali ya Iraq kufanya uchunguzi ili kupata ukweli halisi kuhusu shambulizi hilo. Ofisi ya haki za binadamu pia imekaribisha kuhamishwa kwa wakazi 42 wa kambi hiyo walosalia na kuwapeleka kwenye kambi ya Hurriya, ambayo ipo karibu na mji mkuu wa Baghdad.

Hata hivyo, ofisi hiyo imeelezea hofu yake kuhusu madai kuwa wakazi saba wa zamani wa kambi ya Ashraf, sita kati yao wakiwa wanawake, walitekwa nyara wakati wa matukio ya Septemba 1. Ripoti ambazo hazijathibitishwa zinasema kuwa wanazuiliwa katika eneo ambalo halijatambulika nchini Iraq, na huenda wakarejeshwa Iran kwa lazima.