Dola bilioni 2.5 zachangishwa katika ahadi mpya za kufikia malengo ya kukabiliana na umaskini duniani

23 Septemba 2013

Ahadi za ziada za kupiga jeki ufikiaji wa malengo ya maendeleo ya milenia zimetangazwa leo, na hivyo kufikisha dola bilioni 2.5 katika ahadi mpya, kabla ya tarehe ya ukomo wa malengo ya maendeleo ya milenia.

Waziri wa Uingereza wa Maendeleo ya Kimataifa, Justine Greening, ametangaza mchango mpya wa serikali ya Uingereza kwa mfuko wa kimataifa wa kupiga vita UKIMWI, kifua kikuu na malaria wenye thamani ya dola bilioni 1.6, katika kipindi cha miaka mitatu kati ya 2014 na 2016.

Mchango huo utasaidia katika utoaji wa dawa za kupunguza makali ya Ukimwi kwa watu 750,000 wanaoishi na virusi vya HIV, vyandarua vya kuzuia mbu wasababishao malaria milioni 32, na tiba dhidi ya kifua kikuu kwa watu zaidi ya milioni moja.

Nayo serikali ya Norway imetangaza kuwa itachangia dola milioni 75 katika kipindi cha miaka mitatu ili kufadhili upatikanaji wa vifaa vya kuokoa maisha na gharama za kuvisafirisha, kama sehemu ya Mfuko mpya ulozinduliwa wa afya ya uzazi, watoto wachanga na mama wazazi.

Nao mtandao wa kimataifa Energia, ambao unahusika na nishati endelevu, umahidi zaidi ya dola milioni 10 kusaidia katika kuimarisha juhudi za kuongeza usawa wa kijinsia na upaji nguvu wanawake katika sekta ya nishati.