Tovuti ya kimataifa ya ufahamu yazinduliwa kuimarisha nguvu za wanawake kiuchumi

23 Septemba 2013

Wakati wa kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kitengo cha maswala ya wanawake katika Umoja wa Mataifa, UN Women, kwa ushirikiano na serikali ya Canada, leo wamezindua uwanja wa kimataifa wa kuwapa wanawake ufahamu wa kujiimarisha kiuchumi, ambao utakuwa ni tovuti ya (www.empowerwomen.org).

Uwanja huu wa mafunzo ulo wazi kwenye tovuti, unalenga kuibua tena upaji nguvu za kiuchumi kwa wanawake, kwa kujenga mitandao na kuwaleta pamoja watu wanaoihataji rasilmali na wale walizo nazo.

Wanawake huchangia uchumi kwa kiasi kikubwa kupitia katika biashara, mashambani, kama wajasiriamali na waajiriwa, pamoja na kufanya kazi kubwa isokuwa na malipo ya malezi nyumbani. Wengi walioajiriwa wapo katika sekta zisizo rasmi, na katika ajira zinazowatia hatarini, takriban thuluthi mbili kati yao wakiwa hawalindwi na sheria.

Tovuti hiyo ya www.empowerwomen.org imetokana na ushahidi unaoendelea kujitokeza kuwa kuwekeza katika upaji wanawake nguvu za kiuchumi kunaweka njia ya moja kwa moja ya kufikia usawa wa kijinsia, kutokomeza umaskini na ukuaji wa jumuishi wa kiuchumi.