Maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI miongoni mwa vijana yapungua kwa kiwango kikubwa:UN

23 Septemba 2013

Shirika la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na Ukimwi,UNAIDS limesema kuwa maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi miongoni mwa vijana yamepungua kwa kiwango cha kuridhisha kwa  asilimia 52 huku watu wazima yakipungua kwa asilimia 33. Kupungua huko kumerekodiwa kuanzia mwaka 2001

Takwimu hizo zimetolewa katika wakati ambapo viongozi wa kimataifa wakijaandaa kukutana mjini New York katika Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kujadilia masuala mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya mellenia.

Alice Kariuki na taarifa kamili

TAARIFA YA ALICE KARIUKI

Kiwango cha maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa vijana na watu wazimu kilikadiriwa kufikia milioni 2.3 hadi kufikia mwaka 2012, ikiwa  kimepungua kwa asilimia 33 tangu kipindi cha mwaka 2001.

Kwa upande wa vijana pekee, kiwango hicho kimepungua hadi kufikia 260 000 ikiwa ni sawa na asilimia 5 kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2001.Kumekuwa pia na kupungua kwa vifo vitokanavyo na matatizo ya ukimwi.

 Ripoti zinasema kuwa vifo hivyo vimepungua kwa asilimia 30, tangu mwaka 2005 ambako kulikuwa na idadi kubwa ya watu waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.

Mipango iliyowekwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ni kuhakikusha kwamba ifikapo mwaka 2015 watu wengi wanafikiwa na madawa ya kufubaza nguvu za virusi vya Ukimwi.

Akizungumza na redio ya Umoja wa Mataifa Afisa Mkuu UNAIDS anayehusika na masuala ya data , Peter Ghys alisema kuwa

(SAUTI YA Peter Ghys)

“ Siyo tu kwamba tunaweza kufikia malengo ya mwaka 2015 ya kuwatibu watu milioni 11, lakini pia tunapaswa kwenda mbali ya hapo na kuanisha sera na mikakati ambayo itahakikisha kwamba hakuna mtu anayeachwa nyuma”.