UNHCR yahitaji dola milioni $21.4 zaidi kwa wakimbizi wa DRC walioko Uganda

20 Septemba 2013

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, limesema linahitaji kwa dharura zaidi ya dola Milioni 21.4 kwa ajili ya operesheni zake nchini Uganda ambazo zinakabiliwa na uhaba wa ufadhili, ili kuwasaidia wakimbizi kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Grace Kaneiya na ripoti kamili.

(Taarifa ya Grace)

Kiasi hicho cha fedha kitaweza kukidhi mahitaji ya hadi mwishoni mwa mwaka, na kimebadilishwa hasa kutokana na makumi ya maelfu ya wakimbizi kuingia nchini Uganda kwenye wilaya ya Bundibugyo na maelfu ya wengine kutoka eneo la Kamango, kwenye mkoa wa Kivu ya Kaskazini tangu mwezi Julai. Kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi wanaoingia Bundibugyo kutoka Kivu ya Kaskazini kulianza mwezi Julai, pale ambapo kundi la waasi wa Allied Democratic Forces kutoka Uganda lilipouvamia mji wa Kamango na kukabiliana na majeshi ya serikali ya DRC.Adrian Edwards ni maemaji wa UNHCR

(Sauti ya Adrian)

Ombi letu jipya ni sehemu ya ombi la mashirika la UM lililorekebishwa la jumla ya dola Milioni 92 kwa ajili ya wakimbizi hao wanaoendelea kumiminika kusini kati na kusini-magharibi mwa Uganda. Ofisi ya Umoja wa Mataifa Uganda inajitahidi kuwapatia chakula, vifaa vya misaada na huduma muhimu.”

Kufikia sasa kuna takriban wakimbizi wa ndani milioni 2.6 nchini DRC, huku zaidi ya wakimbizi 290,000 wakiwa wamekimbilia nchi jirani tangu mwanzoni mwa mwaka jana. Nchini Uganda, wakimbizi 170,000 wamepata msaada katika wilaya tatu tofauti.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter