Uridhiaji wa kimataifa wa mkataba wa haki za watoto unahitajika ili kuwalinda:

19 Septemba 2013

Mwakilishi maalumu wa watoto na vita vya silaha Bi Leila Zerrougui na mwakilishi maalumu wa ukatili dhidi ya watoto Marta Santos Pais leo wametoa wito wa kimataifa wa kuridhia mkataba wa haki za mtoto na vipengee vyake vitatu.

Wawakilishi hao wamesema mamilioni ya watoto duniani wanakabiliwa na machafuko, kunyonywa na ukatili. Na kwa kuwa wamepuuzwa na takwimu na hatua za kisera basi wamekuwa ni wahanga wa kimyakimya, wakibaguliwa kwenye mijadala ya jamii.

Wameongeza kuwa watoto wanahitaji ulinzi wa ziada ambao utapatikana tuu kwa kuridhia mkataba wa haki za mtoto na vipengee vyake.

Bi Zerougui amesema kikao maalumu cha mwaka huu kwenye Umoja wa mataifa kinatoa msisitizo na umuhimu wa mkataba wa haki za mtoto na mjadala wa Septemba 24, 25, 26, 30 na tarehe Mosi Oktoba kwenye baraza kuu ni fursa muafaka ya nchi wanachama kutia saini na kuridhia mkataba huo muhimu na vipengee vyake.