Takwimu mpya za UNESCO zadhihirisha jinsi elimu inavyochangia maendeleo

19 Septemba 2013

Iwapo watoto wote wangalipata elimu, mapato ya kila mtu yangaliongezeka kwa asilimia 23 katika kipindi cha miaka 40. Hayo ni kwa mujibu wa takwimu mpya za Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni katika Umoja wa Mataifa, UNESCO. Takwimu za UNESCO zinaonyesha pia kuwa iwapo wanawake wote wangalipata elimu ya msingi, ndoa za watoto na vifo vya watoto vingepungua kwa sudusi moja, na vifo vya akina mama wazazi kwa thuluthi mbili.

Elimu ina uwezo wa kipekee wa kupunguza umaskini wa kupindukia na kuchagiza malengo ya maendeleo kwa ujumla, kulingana na takwimu za ripoti ya UNESCO ya ufuatiliaji wa elimu kwa wote kote duniani, ambayo itatolewa karibuni.

Tathmini hii imetolewa kabla ya mijadala ya Baraza Kuu kuhusu ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015. Takwimu hizo zinaonyesha kuwa kuwekeza katika elimu, hususan ya wasichana, kunasaidia kupunguza umaskini kwa kuchangia faida kubwa katika afya na uzalishaji, pamoja na ujumuishaji katika demokrasia na kuwapa nguvu wanawake.

Hata hivyo, ili kufungua milango ya nguvu za mchango wa elimu, malengo mapya ya maendeleo ni lazima yaende hatua zaidi kuhakikisha kuwa watoto wote wananufaika si tu kwa kupata elimu ya msingi yenye viwango vya juu, bali pia kwa kupata elimu ya sekondari ya viwango vya juu.

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Irina Bokova, amesema ripoti hiyo inathibitisha dhahiri kuwa elimu inaweza kubadilisha maisha na jamii kuwa bora zaidi, na kuongeza kuwa malengo ya elimu duniani ni ajenda ambayo haijakamilika.