Nchi nne za afrika zaafikiana mpango wa udhibiti wa maji:

18 Septemba 2013

Katika juhudi za kuboresha udhibiti wa vyanzo vya maji, mataifa manne ya ya Kaskazini Mashariki mwa Afrika Jumatano yameafikiana kwenye mkutano wa 57 wa shirika la kimataifa la nguvu za atomiki IAEA mjini Vienna, kuanzisha mkakati wa muda mrefu wa utumiaji na udhibiti wa mifumo ya maji. Flora Nducha na taarifa kamili.

(TAARIFA YA FLORA NDUCHA)

Mataifa hayo ambayo ni Chad, Misri, Libya na Sudan yametia saini mpango madhubuti wa kuchukua hatua ujulikanao kama (SAP) ukiwa na lengo la kuongeza matumizi sawa ya mfumo wa chemichemi ya Nubian Sandstone, ambao ni mfumo mkubwa kabisa wa maji unapita chini ya mataifa hayo manne. Makubaliano yao yalitokana na mradi wa pamoja wa ushirikiano wa kiufundi kutoka shirika la Umoja wa mataifa la maendeleo UNDP, kitengo cha kimataifa cha mazingira GEF, shirika la elimu sayansi na utamaduni UNESCO na IAEA. Mkurugenzi mkuu wa IAEA Yukiya Amano amezipongeza nchi hizo nne kwa mafanikio waliyofikia akisistiza kuwa maji ni rasilimali muhimu na udhibiti na matumizi mazuri ya rasilimali hiyo ni kiungo cha mustakhbakli wa baadaye wa maji.