Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kikao cha 68 cha Baraza Kuu chafunguliwa rasmi

Kikao cha 68 cha Baraza Kuu chafunguliwa rasmi

Kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kimefunguliwa rasmi hii leo.

Ni sauti ya rais mpya wa Baraza Kuu, John William Ashe, raia wa Antigua naBarbuda, ambaye atakiongoza Kikao cha 68. Kikao hicho kinaanza kwa mikutano mbali mbali, ambayo kilele chake kitakuwa ni mkutano mkuu wa viongozi wa nchi wanachama mnamo wiki ijayo. Akizungumza wakati wa kukifungua Kikao hicho, Bwana Ashe amesema kauli mbiu ya kikao hicho itakuwa ni: kuandaa jukwaa la ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015. Mwaka ujao utajitokeza kuwa muhimu kwa Baraza Kuu, wakati likijaribu kutambua vipimo vya ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015.

 Ukubwa wa kazi ilioko mbele yetu, itahitaji hatua za dhati na ushirikiano wa hali ya juu. Ni lazima tudhihirishe kuwa juhudi zetu zinalingana na kazi hiyo. Ili kuandaa jukwaa hilo la ajenda ya maendeleo, natarajia kuandaa mijadala mitatu ya ngazi ya juu, ikiwemo mchango wa wanawake, vijana na mashirika ya umma, mchango wa haki za binadamu na uongozi wa kisheria, pamoja na mchango wa mataifa ya Kusini mwa dunia na teknolojia ya mawasiliano katika ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015.

 Akiongea wakati wa ufunguzi wa Kikao hicho cha 68, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema matarajio katika kipindi cha Kikao cha 68 ni mengi, akiongeza kuwa la kuzingatiwa kwanza ni kuongeza kasi ya kufikia malengo ya maendeleo ya milenia, MDGs, wakati ukomo wake ukikaribia mnamo mwaka 2015.

 Jumuiya ya wafanyabiashara, mashirika ya umma na mashirika ya kibinadamu yatakuja pamoja kuonyesha ufanisi wa MDGs. Tutaongeza kasi ya juhudi za kubuni ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015, pamoja na fungu la malengo ya maendeleo endelevu ambayo tunatarajia kuwa yatakabiliana na changamoto kanganishi za nyakati hizi, na kusisimua mawazo ya watu kote duniani, jinsi malengo ya maendeleo ya milenia yalivyofanya.

 Bwana Ban amesema wakati wa Kikao cha 68, maandalizi ya kongamano la mwaka 2014 kuhusu Mataifa Madogo ya Visiwani yanayoendelea, pamoja na mikutano ya Baraza Kuu kuhusu watu wenye ulemavu na uhamiaji, na pia kuangazia changamoto za dharura za amani na usalama, likiwemo suala la Syria.