Baraza Kuu lahitimisha kikao chake cha 67

16 Septemba 2013

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limehitimisha kikao chake cha 67, ambacho kimedumu mwaka mmoja sasa. Kuhitimishwa kwa Kikao cha 67 kunakaribisha kuanza kwa Kikao cha 68, ambacho kilele chake kitakuwa ni mkutano wa viongozi wa kimataifa mnamo wiki ijayo. Joshua Mmali ana maelezo zaidi

(TAARIFA YA JOSHUA)

Kikao cha 67 kiliendeshwa na Bwana Vuk Jeremic, mwanadiplomasia wa Kiserbia ambaye amesema wakati wa kikao hicho, nchi wanachama zilifanya maaumuzi muhimu yapatayo 90, na kupitisha takriban maazimio 300, ukiwemo Mkataba wa Biashara ya Silaha.

Mkataba huo unatarajiwa kuendeleza uwazi katika biashara ya silaha na kuwawajibisha wauzaji kutoa tathmini kuhusu ikiwa biashara zao zinachangia ukiukwaji wa haki za binadamu na sheria ya kibinadamu.

Ametaja pia kura ya kuitambua Palestina kama taifa mwangalizi asiye mwanachama katika Umoja wa Mataifa kama mfano wa ufanisi wa Kikao cha 67, lakini akasema suala la Syria limempa aibu kubwa.

Akizungumza katika mkutano wa leo, Katibu Mkuu Ban Ki-Moon amesema kuwa Kikao cha 67 kimeendeshwa katika kipindi cha changamoto kubwa kwa jamii ya kimataifa.

"Baraza hili liliingilia kati wakati Baraza la Usalama lilikuwa limegawanyika kuhusu Syria. Baraza hili pia liliendelea kukabiliana na athari za muda mrefu za mdororo wa uchumi wa kimataifa."

Nchi wanachama pia zilianza mijadala muhimu kuhusu ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 katika kikao cha 67.