Baada ya ripoti, Baraza sasa latafakari athari na azimio laandaliwa: Rais wa Baraza

16 Septemba 2013

Baada ya kupatiwa ripoti kuhusu matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria, Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa sasa linajikita katika hatua zitakazochukuliwa hususan kupitia baraza hilo, hiyo ni kauli ya Rais wa baraza hilo Balozi Gary Quinlan alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea ripoti ya uchunguzi wa matumizi ya silaha za kemikali kwenye eneo la Ghouta, huko Damascus, Syria.

Balozi Quinlan amesema bila shaka baraza huwa linakuwa na umoja pindi silaha za kemikali zinapotumika mahali popote na wakati wowote na kwamba wanaunga mkono makubaliano ya Urusi na Marekani juu ya uhifadhi na uteketezaji wa silaha za kemikali za Syria. Hata hivyo katika kufanikisha hilo wamefikia makubaliano ya kwamba……

(Sauti ya Balozi)

“Tumekubaliana kuwa azimio ni muhimu kwa mchakato huo na tumekubaliana kuandaa azimio ambalo litajumuisha makubaliano hayo ya mwishoni mwa wiki kati ya Urusi na Marekani. Siwezi kutaja muda kamili wa shughuli hiyo lakini wajumbe wote wanatambua uharaka wake na kama mjuavyo hatua za awali ni kwa serikali mbili zilizokubaliana mwishoni wma wiki kuwailisha rasimu ya uamuzi kwa baraza tendaji la OPCW huko the Hague.”

Halikadhalika amesema ndani ya Baraza kuna azma ya dhati ya kuona mzozo wa Syria unapatiwa suluhu la kisiasa.