Sarin ilitumika Syria Je ni nani alitumia, haikuwa jukumu la Tume: Ban

16 Septemba 2013

Kiwango kikubwa cha kutisha cha kemikali aina ya Sarin kilitumika kwenye shambulio la tarehe 21 Agosti huko Ghouta, kwenye viunga ya mji mkuu wa Syria, Damascus, ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon wakati akiwajulisha waandishi wa habari mjini New York, kile kilichomo kwenye ripoti ya uchunguzi Syria, ambayo aliwasilisha kwa Baraza la Usalama na Baraza kuu siku ya Jumatatu.

Bwana Ban amesema amesikitishwa sana na kitendo hicho ambacho amesema ni uhalifu mkubwa wa kivita ambao ni kinyume na itifaki ya mwaka 1925 na kanuni nyingine za kimataifa. Katibu Mkuu alipoulizwa kuhusu tume imebaini ni nani ametumia silaha hizo, alikuwa na haya ya kusema.

(Sauti ya Ban)

“Ujumbe ulioongozwa na Dokta Sellstrom umeweza kubaini pasi shaka kuwa Sarin ilitumika kwa kiasi kubwa. Kazi ya tume ilikuwa kubaini iwapo silaha za kemikali zimetumika na kwa kiasi gani, na siyo ni nani ametumia. Ni kwa wengine kuamua iwapo wachunguze zaidi kubaini nani anawajibika. Tunaweza kuwa na fikra zetu kuhusu hili lakini naweza kusema kuwa tukio hili lilikuwa ni uhalifu wa kutisha na wahusika wanapaswa wafikishwe mbele ya sheria haraka iwezekanavyo.”

Bwana Ban amesema tume ya Dokta Sellstrom itarejea Syria kukamilisha majukumu yaliyosababisha iundwe mara baada ya Syria kutoa idhini.