Silaha za kemikali zilitumika Syria: Ripoti

16 Septemba 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ripoti ya uchunguzi wa matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria tarehe 21 mwezi uliopita imethibitisha pasipo shaka kuwa silaha hizo zilitumika.

Katika taarifa yake kwa Baraza la Usalama Jumatatu Ban ameelezea kusikitishwa na kiwango kikubwa cha silaha za kemikali kilichotumika na kuleta maafa kwa raia hususan watoto. Amesema katika uchunguzi huo huko Ghouta kwenye viunga vya mji mkuu Damascus ulioongozwa na Profesa Ake Sellstrom, zaidi ya wahanga 50 wa tukio hilo walihojiwa pamoja na wahudumu wa afya na waokoaji.

Amesema matumizi ya silaha za kemikali ni kinyume na itifaki ya mwaka 1925 na kanuni nyingine za kimataifa hivyo amesema ni matumiani yake wajumbe wote wa Baraza la Usalama wataungana naye kulaani kitendo hicho na kwamba jumuiya ya kimataifa ina wajibu wa kuhakikisha silaha za kemikali hazitumiki tena vitani.

Katibu Mkuu amesema umoja ndani ya baraza hilo ni muhimu zaidi hivi sasa kwa kuzingatia hali ilivyo hususan wakati huu ambapo tayari Syria imekubali kuwa inamiliki silaha za kemikali na tayari imekubali kujiunga na mkataba wa kutokomeza silaha hizo.

Hadidu za rejea za uchunguzi huko Ghouta zilitaka tume hiyo kuchunguza iwapo silaha za kemikali zilitumika au la na kuwasilisha matokeo kwa Katibu Mkuu.

Wakati huo huo, Tume hiyo ya Profesa Sellstrom imesema itaendelea kuchunguza madai mengine ya matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria na matokeo ya uchunguzi huo yatawasilishwa mapema iwezekanavyo.