Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bodi ya UNCTAD kujadili njia mwafaka za kukabiliana na mdororo wa kiuchumi

Bodi ya UNCTAD kujadili njia mwafaka za kukabiliana na mdororo wa kiuchumi

Bodi ya usimamizi ya Kamati ya Biashara na Maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD, inakutana kujadili jinsi ya kuzisaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na hali ya wasiwasi ilosababishwa na mdororo wa kiuchumi.

Mkutano huo wa wiki mbili umeanza leo Jumatatu kwa hotuba ya Mkurugenzi Mkuu mpya wa UNCTAD, Mukhisa Kituyi. Bwana Kituyi ambaye ni raia wa Kenya, alichukuwa wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa saba wa UNCTAD mnamo Septemba mosi.

Miongoni mwa masuala yanayojadiliwa na bodi hiyo ni jinsi ambavyo UNCTAD inatakiwa kuendeleza mienendo mipya ya ukuaji katika biashara na maendeleo, ushirikiano wa kiuchumi, mchango wa ununuzi wa kitaifa na kikanda katika kufikia ukuaji endelevu wa kiuchumi.

Mengine muhimu ni mchango wa mitandao ya kimataifa ya kuongeza thamani ya bidhaa, maendeleo ya kiuchumi barani Afrika, juhudi za kuzisaidia nchi maskini na msaada kwa watu wa Palestina.